Kenya: Nairobi yapata gavana baada ya Sonko kuenguliwa

Sakaja sasa anakuwa gavana wa nne wa Nairobi na wa tatu kuchaguliwa na wakaazi; mpinzani wake Polycarp Igathe amekubali matokeo

0

Wakaazi wa kaunti ya Nairobi mji mkuu wa Kenya wamepata nafasi ya kumchagua gavana mwingine baada ya aliyekuwa gavana wa pili Mike Mbuvi Sonko kutemwa na bunge la kaunti ya Nairobi mwaka 2020. Sonko alienguliwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ya gavana na kukiuka katiba katika kutekeleza kazi yake.

Gavana mteule wa Nairobi Johnson Sakaja akipokea cheti baada kutangazwa mshindi

Senate wa jimbo hilo la Nairobi anayeondoka Arthur Johnson Sakaja ambaye alikuwa anawania kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) ametangazwa kuwa gavana mteule baada ya kupata kura 699,392 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Polycarp Igathe ambaye alipata kura 573,516. Igathe ambaye amewania na chama cha Jubilee. Katika kinyang’anyiro hicho, utafiti wa kura ya maoni umekuwa ukimuorodhesha Sakaja kuwa mbele ya Igathe ambaye aliwahi kuwa naibu gavana wakati wa Sonko japo akajiuluzu baada ya miezi tatu. Sakaja mwenye umri wa miaka 37 hata hivyo amekabiliwa na vizingiti si haba ikiwemo madai kwamba hana stakabadhi za masomo. Sakaja sasa anakuwa gavana wa nne wa Nairobi na wa tatu kuchaguliwa na wakaazi. Tayari mpinzani wake Polycarp Igathe amekubali matokeo na kumpongeza Sakaja kwa kushinda katika uchaguzi huo.
“Nakubaliana na uamuzi wa wakaazi wa Nairobi na kuwashukuru wafuasi wangu kwa kusimama na mimi. Gavana wa Nairobi ni Johnson Sakaja,” amesema Igathe katika mtandao wa Twitter. Naye Sakaja akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti chake, amewahidi wakaazi kutekeleza wajibu wake kama gavana jinsi alivyosema wakati wa kampeni. Kitumbua katika kaunti ya Nairobi kiliingia mchanga mwaka 2020, gavana Mike Sonko gavana wa wakati huo alipomteule Ann Kananu kama naibu gavana kujaza nafasi ya Polycarp Igathe ambaye alikuwa amejiuzulu. Hata hivyo, mkaazi mmoja aliwasilisha kesi mahakamani kupinga kuteuliwa kwa Kananu hali iliyopelekea kusalia nje hadi Disemba mwaka 2020 hadi Sonko alipoenguliwa na kesi dhidi yake kutupiliwa mbali. Baada ya hapo Kananu alipigwa msasa, akaidhinishwa na kuapishwa kama naibu gavana na alipokuwa anajianda kuapishwa Sonko alirejea mahakamani japo ombi lake likatupiliwa mbali. Wakati wote huo spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Benson Mutura ndiye alikuwa anashikilia ugavana. Kulingana na kipengele cha 182 ibara ya 2-4 cha katiba ya Kenya, spika wa kaunti atachukua nafasi ya ugavana iwapo gavana atafariki au kuondolewa ofisini na naibu wake hawezi kuchukua nafasi hiyo.

Seneta mteule wa Nairobi Edwin Sifuna

Viongozi wengine ambao wamechaguliwa ni katibu mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna ambaye ametangazwa kuwa Senate wa Nairobi. Sifuna amepata kura 716,651 dhidi ya Bishop Margaret Wanjiru wa United Democratic Movement (UDA) ambaye amepata kura 524,091.

Mwakilishi wa kike wa Nairobi Esther Wanjiru Passaris

Na mwakilishi wa akina mama Esther Passaris amefanikiwa kutetea kiti chache. Passaris amepata kura 698,929 na kumshinda Milicent Omanga wa UDA ambaye amepata kura 586,246. Tayari Omanga amekubali matokeo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted