Rais Samia awaonya viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuchochea chuki kisiasa
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema tofauti za kisiasa au mapenzi binafsi kwa kiongozi haziwezi kuwa sababu ya kuvuruga amani ya nchi, akisisitiza kuwa Tanzania imejengwa katika misingi ya demokrasia na utulivu tangu kuanzishwa kwake.
Akihutubia wazee wa Dar es Salaam leo, Rais Samia amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha huduma za jamii na uchumi, na kwamba wanaoeneza chuki dhidi yake hawapaswi kutumia misingi ya dini au ukabila kuibua mgawanyiko.
“Hata kama aliyepo juu ya Serikali humtaki, kuna muda. Hii ni nchi ya kidemokrasia; huyu mtu ataongoza hadi kipindi hiki. Kama amefanya kosa, lisemeni kosa la kuongeza huduma bora za afya? Au kujenga mashule mazuri? Au kukuza uchumi hadi kusifiwa duniani? Kosa letu ni nini?” alihoji.
Ameongeza kuwa kutopenda kiongozi hakupaswi kuwa kichocheo cha vurugu: “Kama mtu hampendi anayeongoza, tustahimili tu. Ataongoza, ataondoka. Wote walioongoza tangu awamu ya kwanza, je, wote walipendwa? Kulikuwa na vurugu? Kama haumpendi Samia kwa sababu ya dini yake au alikotoka, hakuna sababu ya kuvuruga nchi.”
Rais Samia pia aliwaonya wananchi dhidi ya kile alichokiita “sumu za kisiasa” zinazoenezwa kwa jina la dini, akisema mbinu hizo hujenga chuki na kuharibu umoja wa taifa.
“Niwaombe sana: zile sumu zinazotiwa huko, mnapotiwa sumu tumieni akili zenu. Hakuna eneo baya la kumpata mtu kama dini; ukimlisha ubaya unajenga chuki moyoni. Wanasiasa wanamuharibu mtu kichwani,” alisema.
Katika wito mahsusi kwa viongozi wa dini, Rais Samia aliwahimiza kudumisha misingi ya maadili na kushikilia nafasi yao kama walinzi wa amani ambapo moja kwa moja alilitaja Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), ambao mara kadhaa wamekuwa wakitoa waraka mzito dhidi ya mamlaka.Rais Samia alisema baraza hilo limekuwa likitoa matamko mara kwa mara, ikiwemo manane yaliyotolewa katika kipindi kifupi. Hata hivyo, amesema hata ndani ya TEC kuna viongozi wanaopinga matamko hayo wakiyaita batili, jambo analosema linaonesha kuwa msimamo huo si wa taasisi nzima.
“Viongozi wa dini kaeni kwenye mstari wenu. Dini zetu zote zinasema mamlaka yote yamewekwa na Mungu iwe mwanamke au mwanaume. Mungu ndiye anajua kwa nini Samia yupo hapa. Majoho yenu yaoneshe sura halisi. Hakuna kitabu cha dini kilichosema kitumie dini kuvuruga nchi,” alisisitiza.
Amehitimisha kwa kuwataka viongozi wa kidini na wananchi wote kulinda umoja wa kitaifa na kuepusha misuguano inayoweza kuhatarisha amani ya Tanzania.