Mitandao ya kijamii hubanwa na kudhibitiwa barani Afrika, vipi na kwanini?

Mara nyingi kampuni zinazotoa huduma za mtandao haziwezi kukataa maagizo ya serikali zao kubana au kuzima mitandao.

0

Asilimia 60 ya idadi ya watu wote duniani takriban 4.66 bilioni hutumia mtandao, ikiwa ni chanzo cha taarifa za papo hapo, burudani, habari na mwingiliano wa kijamii  na njia rahisi ya kupata habari na burudani.

Ila unafahamu kuwa kuna nchi ambazo utumizi wa mtandao umebanwa na hata kupigwa marufuku?

Kunako nchi ambako mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook, Instagram imebanwa, vyombo vya habari na hata matangazo ya kisiasa.

Kutokana na kuwepo kwa vizuizi na sheria kali,uhuru wetu mtandaoni upo hatarini zaidi kuliko hapo awali.

Nchi ambazo zinaongoza kwa udhibiti wa mtandao ni China na Korea Kaskazini. Raia katika nchi hizi wamewekewa marufuku ya kutumia mitandao yote, kutazama baadhi ya filamu na hata kutumia VPN. Vyombo vyote vya habari vya kisiasa vinavyochapishwa katika nchi hizo vinakaguliwa na serikali. Mitandao ya kijamii inayoruhusiwa ni ile iliyobuniwa katika nchi hizo na hudhibitiwa na serikali, mfano China hutumia mtandao wa WeChat uliobuniwa nchini humo.

Nchini Iran utumizi wa VPN umebanwa na mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Instagram na YouTube imepigwa marufuku ikiwemo ponografia, huku vyombo vya habari vya kisiasa vikikaguliwa. Qatar, Belarus, Turkmenistan,Syria na Falme za Kiarabu, nchi zote hizi zimepiga marufuku ponografia, zimedhibiti vyombo vya habari vya kisiasa na kuzuia mitandao ya kijamii.



53% – 81% ya nchi barani Afrika hudhibiti vyombo vya habari huku Algeria,Cameroon na Chad wakikandamiza maoni ya kisiasa katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii. 60% ya mataifa ya Afrika yameweka vikwazo tofauti katika utumizi wa mitandao ya kijamii , Eritrea ikiwa imebana sana utumizi wa mitandao ya kijamii. Misri ni taifa la pekee kuzuia kabisa utumizi wa VPN ingawaje utumizi wa VPN ni halali.

Katika mataifa ya Afrika utumizi wa mtandao na mitandao ya kijamii hubanwa mara nyingi wakati wa uchaguzi. Uganda ikiwa taifa la hivi karibuni kubana matumizi ya mtandao wakati wa uchaguzi mkuu Januari 14 2021. Wanaharakati wa haki za kidijitali wanasema ni udhibiti, lakini serikali zinahoji kuwa inasaidia kudumisha usalama.

Si Uganda pekee iliyobana matumizi ya mtandao, Tanzania pia ilibana matumizi ya mtandao na mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi wa 2020. Mwezi Juni mwaka wa 2020, Ethiopia pia iliweka kizuizi kwa utumizi wa mtandao iliyodumu mwezi mmoja baada ya mwanaharakati na msanii maarufu kutoka jamii ya Oromo Hachalu Hundessa kuuawa.

Nchi za Zimbabwe, Togo, Burundi, Chad, Mali na Guinea pia ziliweka vizuizi kwa utumizi wa mtandao mwaka huo.

Mara nyingi kampuni zinazotoa huduma za mtandao haziwezi kukataa maagizo ya serikali zao kubana au kuzima mitandao kwasababu kampuni hizo hupewa leseni za kuendesha shughuli zao na serikali, hii ina maana kwamba iwapo watakataa watakuwa kwenye hatari ya kutozwa faini au kupoteza kandarasi zao.

Wenye kampuni za kutoa huduma za mitandao wanaweza kukata rufaa mahakamani lakini mara nyingi hawafanyi hivyo.

Hata baada ya mtandao kubanwa au kudhibitiwa kuna njia tofauti ambazo mtu anaweza kutumia ili apate mtandao, njia inayotumiwa na wengi ni VPN ambayo si rahisi kudhibitiwa. Serikali pia zinaweza kuzuia VPN, ila hawafanyi hivyo kwasababu mabalozi, wanadiplomasia na kampuni kubwa hutumia sana VPN kwa kuwa ni salama.

Baadhi ya serikali za Afrika zimetaja ongezeko la habari feki mtandaoni kama sababu ya kutekeleza vikwazo, lakini baadhi ya wachambuzi na wanaharakati wanaona hiki kuwa kisingizio cha kukandamiza makundi yanayoikosoa serikali.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted