Wanajeshi wa Burkina Faso wakosolewa na mataifa mengine lakini waungwa mkono nchini mwao

Mamia ya watu walikusanyika katika uwanja wa Nation Square kusheherekea kung'olewa madarakani kwa Rais Kabore

0
Wanajeshi wa MPSR walioongoza mapinduzi Burkina Faso (Picha AFP)

Wafuasi wa serikali mpya ya Burkina Faso walifanya maandamano siku ya Jumanne huku Umoja wa Mataifa, Ufaransa na majirani wakilaani mapinduzi  ya hivi punde.

Maafisa wa jeshi walimzuilia Rais Roch Marc Christian Kabore siku ya Jumatatu huku kukiwa na hasira kali kutokana na jinsi alivyoshughulikia uasi wa kijihadi.

Nchi hiyo sasa iko mikononi mwa Vuguvugu la Patriotic for Preservation and Restoration (MPSR), jina la junta linaloongozwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba.

Mamia ya watu walikusanyika katika uwanja wa Nation Square katikati mwa mji mkuu Ouagadougou, wakipeperusha bendera na kupiga honi za vuvuzela katika onyesho kubwa la kuunga mkono jeshi, huku wachuuzi waliokuwa karibu wakiuza mabango ya mwanajeshi huyo aliyemng’oa rais madarakani.

“Tulitoa wito wa kuondoka kwa Rais Kabore mara kadhaa, lakini hakutusikiliza. Jeshi lilitusikia na kuelewa,” alisema Lassane Ouedrago, mwanaharakati katika kundi la mashinani.
“Kulingana na sisi, sio mapinduzi,” Julienne Traore, mwalimu mwenye umri wa miaka 30 alisema.
“Ni ukombozi wa nchi, ambayo ilikuwa inatawaliwa na watu ambao hawakuwa na uwezo.”

Baadhi ya waandamanaji walibeba bendera za Mali na Urusi — rejeleo la jeshi la kijeshi la nchi jirani ya Mali, ambalo mwaka 2020 pia lilichukua madaraka kutokana na maandamano ya kupinga umwagaji damu wa wanajihadi, na hivi karibuni limeanzisha uhusiano wa usalama na Moscow.
Wanamapinduzi waliongoza mapinduzi Jumatatu walivunja katiba ya Burkina Faso, serikali na bunge na kufunga mipaka ya nchi.

“MPSR itaanzisha tena “uongozi wa kikatiba” kwa wakati unaofaa,” junta ilisema katika taarifa, na kuongeza kuwa amri ya kutotoka nje usiku itatekelezwa.
Siku ya Jumanne, serikali ya kijeshi ilitangaza kurejesha usafiri wa anga huku ikifungua tena mipaka ya nchi kavu kwa magari yanayobeba bidhaa muhimu za rai ana za kijeshi.
Licha ya msukosuko wa kisiasa, maisha mjini Ouagadougou yalionekana kuendelea kama kawaida.
Soko kuu la jiji hilo, maduka na vituo vya petroli vilikuwa wazi, na hakukuwa na jeshi maalum katikati mwa jiji hilo, mwandishi wa habari wa AFP alisema.

Hali tete Afrika Magharibi
Afrika Magharibi imekumbwa na mapinduzi matatu ya kijeshi katika kipindi cha chini ya miezi 18, yakianza na Mali mwezi Agosti 2020, kisha Guinea Septemba 2021.
Hiki ndicho kipindi cha hivi punde zaidi cha msukosuko wa kisiasa kuikumba Burkina Faso, ambayo imekuwa na misukosuko tangu kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Ufaransa mnamo 1960.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikashifu mapinduzi akisema “hayakubaliki”, akisema “jamii za kidemokrasia ni thamani ambayo lazima ihifadhiwe.”
“Jukumu la jeshi lazima liwe kulinda nchi zao na watu wao, sio kushambulia serikali zao na kupigania madaraka,” alisema.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alilaani mapinduzi hayo na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa rais aliyepinduliwa.
Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, ambayo inajumuisha Burkina, ilifanya mkutano maalum, ikalaani mapinduzi ahyo.
Uingereza na Afrika Kusini pia zilipinga mapinduzi hayo.

G5 Sahel,ni muungano wa kupinga jihadi unaojumuisha Chad, Mali, Mauritania na Niger, nao pia umekosoa kile ilichokiita “jaribio la kuvuruga utaratibu wa kikatiba” katika nchi mwanachama wake wa tano Burkina Faso.

Televisheni ya Taifa RTB ilichapisha barua iliyoandikwa kwa mkono kwenye mtandao wa kijamii Jumatatu ambayo iliyodaiwa kuandikwa na Kabore, na kusema kuwa anajiuzulu “kwa ajili ya maslahi ya taifa.”
Barua hiyo haikuweza kuthibitishwa kama kweli imeandikwa na Kabore lakini ECOWAS ilithibitisha kwamba Kabore alijiuzulu, baada ya vitisho na shinikizo kutoka kwa wanajeshi baada ya siku mbili za maasi.
Kabore, Waziri Mkuu Lassina Zerbo na maafisa wengine wakuu serikalini hawajulikani walipo.

Kabore alipinduliwa baada ya hasira kali kutokana na kushindwa kwa serikali kukomesha mzozo wa usalama nchini Burkina Faso.
Wapiganaji wa Kiislamu wenye silaha walianza kufanya mashambulizi na kuvuka mpaka kutoka Mali mwaka 2015, na kuwakabili wanajeshi wa nchi hiyo wenye mafunzo duni na wenye vifaa dhaifu.

Takriban watu 2,000 wamekufa, kulingana na takwimu za AFP. Katika nchi yenye watu milioni 21, takriban watu milioni 1.5 ni wakimbizi wa ndani, kulingana na shirika la dharura la kitaifa CONASUR.
Mashambulizi na umwagaji damu dhidi ya jeshi, polisi na wanamgambo wa kiraia waliojitolea yaliongezeka katika mwaka wa 2021,  uzembe au kutojali kwa makamanda wakuu zilizua hasira kati ya raia.
Siku ya Jumamosi, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano yaliyopigwa marufuku, na kuwakamata makumi ya watu.

Siku iliyofuata, wanajeshi walianza kufanya uasi katika kambi nyingi, na Kabore akapinduliwa Jumatatu.
Kabore alichaguliwa mwaka wa 2015, akijiweka kama kiongozi bora baada ya utawala wa muda mrefu wa Blaise Compaore, ambaye aliingia mamlakani mwaka wa 1987.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted