Jeshi lililoongoza mapinduzi Burkina Faso linataka kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa

Burkina Faso inaungana na nchi nyingine mbili za ECOWAS -- Mali na Guinea -- ambapo kumekuwa na mapinduzi katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

0
Mwanajeshi aliyeongoza mapinduzi Paul-Henri Sandaogo Damiba (Photo by Radiodiffusion Télévision du Burkina / AFP)

Kiongozi wa jeshi lilioongoza mapinduzi nchi  Burkina Faso alitoa wito kutaka kuungwa mkono na jumuiya ya  kimataifa kabla ya mkutano wa kilele wa kikanda ambao unaweza kuiwekea Burkina Faso vikwazo.

“Burkina Faso inahitaji washirika wake wa kimataifa zaidi sasa” Paul-Henri Sandaogo Damiba alisema katika televisheni siku chache baada ya kuongoza kupinduliwa kwa rais Roch Marc Christian Kabore.

“Ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono nchi yetu ili iweze kuondokana na mgogoro huu haraka iwezekanavyo.”

Wakuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wanatarajiwa kujadiliana Ijumaa kuhusu jinsi ya kujibu mapinduzi ya kijeshi ya Jumatatu.

Kabore alitimuliwa madarakani na wanajeshi waasi kutokana na hasira ya umma kwa kushindwa kwake kukomesha ghasia za wanajihadi zinazoliangamiza taifa hilo kubwa la Afrika Magharibi.

Mapema Alhamisi, takriban viongozi 20 wa vyama vya wafanyakazi walikutana kwa takriban nusu saa na junta katika ofisi ya rais katika mji mkuu wa Ouagadougou.

Damiba “alituhakikishia kwamba tutashauriwa na kujumuishwa katika kile kitakachoamuliwa,” alisema Marcel Zante, anayeongoza shirikisho la vyama vya wafanyakazi 130.

“Sasa tunasubiri kuona nini kitatokea,”aliongeza.

Damiba, 41, ni mwanajeshi anayeongoza eneo la mashariki ambalo limeathiriwa pakubwa na wanajihadi.

Siku ya Jumatano, alikutana na baraza la mawaziri wa serikali ya Kabore, ambayo kama bunge limevunjwa.

Jeshi hilo pia limesimamisha katiba, na kuahidi kuweka upya “utaratibu wa kikatiba” ndani ya “wakati unaofaa”

Damiba aliwataka mawaziri wasiondoke nchini bila kibali, na pia alisema anatumai kujumuisha nchi yote katika usimamizi wa kipindi cha mpito, vyanzo vya kisiasa viliiambia AFP.

Mapinduzi hayo ni machafuko ya hivi punde zaidi kuikumba Burkina Faso, nchi ambayo imekumbwa na misukosuko tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.

Siku ya Jumanne, ECOWAS ilitoa taarifa na kusema kuwa umoja huo “unalaani vikali” mapinduzi hayo, ikishutumu jeshi kwa kumlazimisha Kabore kujiuzulu.

Burkina Faso inaungana na nchi nyingine mbili za ECOWAS — Mali na Guinea — ambapo kumekuwa na mapinduzi katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Nchi hizo mbili hazishirikishwi katika shughuli za jumuiya hiyo ya mataifa 15, ambao pia umeweka vikwazo dhidi yao, ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya watu binafsi.

Clement Sawadogo, naibu mkuu wa chama cha Kabore People’s Movement for Progress (MPP), alisema “watawala wanapaswa kufanya kila wawezalo kuzuia vikwazo vya kimataifa kwa Burkina Faso.”

Alitoa wito wa kupatikana kwa suluhisho la busara, kuzuia mzozo unaoendelea wa usalama.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted