Bashe:Serikali haiwezi kutangaza wazi kuwa inazuia usafirishwaji nje ya nchi bidhaa fulani 

Asema kufanya hivyo si jambo jema kwenye biashara, kwa kuwa kuna miongozo ya kanuni za kibiashara.

0
Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo nchini Tanzania

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe amesema serikali haiwezi kutangaza wazi kuwa inazuia usafirishwaji nje ya nchi bidhaa fulani kwa sababu kwa kufanya hivyo si jambo jema kwenye biashara.

Bashe ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole, ambaye alitaka kujua serikali ina mpango gani juu ya kuzuia usafirishwaji wa madini ya phosphate nje ya nchi ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa mbolea.

Katika swali lake kwa wizara ya Kilimo Polepole ameuliza, kutokana na madini hayo kupatikana Tanzania na Australia pekee, je, serikali haioni haja ya kuyabakiza nchini ili yatumike kuzalisha mbolea ya kutosha kwa wakulima

Akijibu swali hilo Waziri Bashe Amesema, “Kama nchi tunaongozwa na kanuni za biashara za WTO, kwa hiyo kutangaza wazi kwamba tunazuia kusafirisha nje ya nchi, sidhani kama misingi ya kibishara ni jambo jema,”

Aidha, ameeleza kuwa serikali imefanya upembuzi yakinifu  kujua kiasi cha phosphate kilichopo nchini na pia inao utaratibu wa kuruhusu kiasi cha madini hayo kinapohitajika kwenda nje ya nchi.

“Haturuhusu export [usafirishaji nje ya nchi] ya holela katika phosphate,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa kuna mwekezaji wa kiwanda cha mbolea mkoani Dodoma ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji Februari 2023, watasimamia rasilimali hiyo kwa maslahi ya wakulima wa ndani ili wapate mbolea ya kutosha, bila kuathiri biashara na nchi nyingine.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted