Jumba la maonyesho Ukraine, lililowapa hifadhi zaidi ya raia 1,000 lalipuliwa kwa mabomu

Zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mji huo wa Mariupol kulingana na mamlaka ya Ukraine.

0

Ukraine ilidai Alhamisi kuwa Urusi iliharibu jumba la maonyesho lenye watu zaidi ya elfu moja katika mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol, na idadi ya waliouawa bado haijajulikana.

Maafisa walichapisha picha ambazo zilionekana kuonyesha jumba la maonyesho la ghorofa tatu  likiwa na shimo na lililokuwa likiteketea moto, huku matofali yakiwa yamerundikana juu.

“Wavamizi waliharibu Ukumbi wa Kuigiza. Mahali ambapo zaidi ya watu elfu moja walipata kimbilio. Hatutawahi kusamehe hili,” Halmashauri ya Jiji la Mariupol ilisema katika chapisho la Telegram.

Siku chache kabla ya shambulio hilo, picha za satelaiti — zilizotolewa na kampuni ya kibinafsi ya Maxar — zilionyesha wazi maneno “DETI” — au watoto kwa lugha ya Kirusi — yakiwa yamechorwa ardhini kila upande wa jengo.

Meya wa Mariupol Vadym Boichenko alitaja shambulio hilo kuwa “janga la kutisha.”

“Watu walikuwa wamejificha huko. Na wengine walisema walikuwa na bahati ya kuishi,” alisema kwenye ujumbe wa video.

“Neno pekee la kuelezea kile ambacho kimetokea leo ni mauaji ya halaiki, mauaji ya halaiki ya taifa letu, watu wetu wa Ukraine. Lakini nina imani kwamba siku itakuja ambapo mji wetu mzuri wa Mariupol utafufuka kutoka kwenye magofu haya.”

Mji huo ni lengo kuu la kimkakati kwa Moscow,ikilenga kuunganisha vikosi vya Urusi huko Crimea upande wa magharibi na Donbas upande wa mashariki na kuzuia Ukraine kufikia kwenye Bahari ya Azov.

Kwa siku kadhaa vikosi vya Urusi vimeshambulia mji huo — ambao wakati mmoja ulikuwa na wakazi wapatao nusu milioni — wakikata umeme, chakula na maji.

Maafisa wa Ukraine walitaja shambulio hilo kuwa uhalifu wa kivita.

“Haiwezekani kupata maneno ya kuelezea kiwango cha ukatili, ambao wavamizi wa Kirusi wanaharibu maisha ya wakazi  wa mji wa Ukraine wa Mariupol,” taarifa rasmi ilisoma.

Mykhailo Podolyak, mshauri wa Rais Volodymyr Zelensky, alishutumu “ukatili” wa Urusi na kuwakejeli viongozi wa Magharibi waliokataa kuweka la eneo lisilo ruka ndege kwa “hofu ya Vita Vya Tatu vya Dunia” na Urusi, huku wakiendela na shughuli zao za kawaida.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilikanusha kuwa vikosi vyake vililipua mji huo na kusema kuwa jengo hilo liliharibiwa na mlipuko uliotekelezwa na kikosi cha waasi cha Azov cha Ukraine.

Ilidai “raia wenye amani wanaweza kushikiliwa mateka” kwenye eneo hilo.

Moscow tayari imelaumu kitengo cha kijeshi kwa shambulio la bomu la wiki jana katika hospitali ya kujifungulia kina mama huko Mariupol, ambalo lilizua malalamiko ya kimataifa.

Mashirika ya haki za binadamu yalisema hali halisi ya Mariupol bado haijafahamika.

“Hadi tutakapojua zaidi, hatuwezi kuondoa uwezekano wa kulengwa na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la ukumbi wa maonyesho lakini tunajua kwamba jumba hilo la maonyesho lilikuwa na takriban raia 500,” Belkis Wille, wa Human Rights Watch alisema.

Zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mji huo uliozingirwa, kulingana na mamlaka ya Ukraine.

Wakazi wanaokimbia mji huo wamezungumza kuhusu miili iliyoachwa kuoza barabarani,.

Vikosi vya Urusi siku ya Jumatano vililenga kituo cha reli katika mji wa Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine, ambapo maelfu ya wakimbizi kutoka Mariupol walikuwa wakijaribu kutoroka mbali zaidi na mapigano.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted