Miaka Miwili ya Rais Samia dhidi ya Wafugaji

Miaka Miwili ya Rais Samia Kwa Jamii ya kifugaji imekua ni kilio badala ya Furaha, tumenyanyaswa na kuumizwa na serikali yetu wenyewe

0

Salaam sana Watanzania wenzangu, Hongereni kwa majukumu ya kila uchao ambayo mnayafanya Kwa ajili ya Taifa letu!

Serikali inaingia madarakani ili kuwajibika kwa ajili ya wananchi wake, ili kuwaletea maendeleo wananchi wake, ili kuondosha Umaskini, Ujinga na Maradhi kwa watu wake na haya yakitekelezwa na serikali basi ndipo kusema inawajibika kwa wananchi wake.

Katika hili pia, utawala wa sheria, haki za wananchi na utawala bora yakiwa ni nyenzo muhimu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo pasipo ubaguzi au upendeleo. Serikali ikijenga vituo vya Afya pasipo kuwepo kwa dawa, vifaa tiba na wataalam ni kazi bure. Ikijenga shule pasipo kuwa na walimu, nyenzo za kufundishia, nyenzo wezeshi (madawati) ni kazi bure.

Ikiwa bado tupo katika kipindi cha mgao wa maji hasa katika majiji makubwa licha ya kubarikiwa kuwa na mito na maziwa makubwa bado ni serikali iliyokosa fikra na ambayo haikusudii kuwaletea wananchi wake maendeleo

Miaka miwili ya Rais Samia; wapo wengi wanaopongeza kwa pengine mazuri wanayoyaona na wapo pia ambao bado wana maumivu makubwa mioyoni mwao pengine kutokana na waliowahi kupitia/kupitishwa na ambayo bado wanaendelea kupitishwa

Na kwamba miaka Hii miwili ya Rais Samia ni ya jasho na machungu kwao kuliko yalivyo kicheko na furaha kwa wafanyabiashara, wanasiasa baada ya kile kinaaminishwa kurejea Kwa Demokrasia na kwa baadhi ya Makundi Mengine ambayo maslahi yao yameboreka,

Wapo wenye machungu kama wakulima kwa kukosa mbegu, waliopoteza ndugu zao baada ya kushikiliwa kwenye vituo vya Polisi, wafanyabiashara wadogo wadogo (maarufu wamachinga) ambao katika maeneo mengi wameondolewa kwenye maeneo yao ya kufanyia biashara na/au vibanda vyao kuchomwa moto na wapo wanaoendelea kuumia kutokana na sheria kandamizi yaliyopo

Miaka hii miwili ya Rais Samia wwa wafugaji yamekuwa ni miaka ya jasho, yaliyojawa na uonevu mkubwa, machungu ya kufungwa, kuwekewa vikwazo vya kimaendeleo na kufanywa maskini na Serikali yake

Kwa Tarafa ya Ngorongoro yapo mambo mengi yanayohatarisha ustawi wa watu wake ambayo kimsingi yameletwa na kusababishwa na serikali yake. Aidha Ngorongoro imekuwa Ngome ya CCM chama dola Kwa miaka yote na ni bahati mbaya kwamba machungu na magumu yote wanayopitia watu wa Ngorongoro yanatokana na serikali ya CCM Kwa miaka yote, Yapo machungu yaliyoasisiwa na serikali zilizopita ( Awamu zilizopita) na yapo ambayo Rais Samia na Serikali yake imeyasababisha!

Mwezi mmoja baada ya Rais Samia kuapishwa, siku akiwa anawaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali alisema hadharani kwamba Ngorongoro wananchi wanaoishi wanastahili kuondolewa kwa kile alichosema ni kutokana na ongezeko la watu, mifugo kuongezeka na kwamba uhifadhi utaharibiwa. Hii imetokana na ripoti ambayo haikuwa shirikishi na kwamba wawakilishi wa Jamii hawakujumuishwa katika kamati iliyokuwa inaratibu kukusanya maoni ya dhidi ya Mapitio ya Matumizi ya Ardhi Mseto Ngorongoro. Ripoti ile ilivuja na moja kati ya mapendekezo ni kuwa watu waondolewe Ngorongoro na kisha kuigawa Ngorongoro katika zone tano ( itakayokuwa kwa ajili ya uwindaji, utalii wa picha, uwekezaji wa mahoteli, eneo dogo hasa maeneo yasiyo na maji yaliyo kame ndipo wananchi wawepo, wengine wote waondolewe ( takriban wananchi sabini elfu ndio waondolewe) ! Rais Samia tarehe 06.04.2021 alipata kukubaliana na wahifadhi kwamba Wamasai wanastahili kuondolewa

Tarehe  21- 25/09/2021 vijana wachungaji walikamatwa wakiwa machungani , walichapwa na baadae mifugo kukamatwa na kudaiwa kulipa Faini ya 18,000,000/=

Tarehe 17/02/2022 Waziri Mkuu alifanya mkutano na wenyeji wa Ngorongoro katika ofisi za NCAA baada ya kushindwa kufika kwenye kikao cha wananchi eneo ambapo wananchi waliiandaa kwa ajili ya Mkutano huo , Kwenye kikao hicho vijana wasomi wa Kimasai walikamatwa, ilikuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia kwenye kikao hicho na simu/laptop na vifaa vya kitamaduni/kimila. Watu walikaguliwa na maafisa usalama! Hata hivyo ofisi ya Waziri Mkuu ilienda kuedit Taarifa ile na kuonesha kwamba  Wananchi wameridhia mpango wao haramu, baadaye waandishi wa habari wa Jamii walikamatwa

Tarehe 24/04/2022 Waandishi wa habari walianza kutumika kufanya spinning dhidi ya wananchi wasio na hatia (waliitwa majina yote mabaya ili tu kuhalalisha watu kuondolewa)

Tarehe 28/05/2022 Msemaji wa Serikali alipata kusema kwenye mtandao wa Clubhouse kwamba serikali imeshauriwa na wadau mbalimbali kusitisha huduma ya miradi ya maendeleo Ngorongoro ili wamasai waondoke na hata hivyo miezi miwili nyuma (13/03/2022) wananchi wa Ngorongoro waliwekewa vikwazo  ya maendeleo- Jumla ya Fedha 2,041,000,000- Billion Mbili na Million arobaini na Moja yalihamishwa kutoa kwenye account (Shule za Msingi/sekondari, Miradi ya Maji na Afya ) yalihamishwa na kupelekwa Handeni

December 2021 wananchi waliripoti uwepo wa chumvi yenye sumu ambayo hutolewa na NCAA baada ya katazo la kupeleka mifugo bonde la Crater Kwa ajili ya kupata madini joto na baadae January 2021 Chumvi ilibainika kuwa na sumu baada ya kupelekwa sampuli kwenye maabara ya mifugo DSM, Chuo cha Mifugo SUA, TBS – wananchi waliripoti mifugo wengi kufa kutokana na chumvi hiyo

Katika uongozi wa Rais Samia 10/05/2022, ndugu zetu wamasai waliokuwa wanafanya kazi NCAA waliandikiwa barua za kuondolewa na kuhamishiwa maeneo mengine ikiwa ni sababu kwamba ndio wanafanya vikao na wananchi ili wasiondolewa kwa nguvu na kuhamishiwa maeneo mengine. Hii sio sawa kama ingefanyika kwao na kwa watoto wao. Kwa sasa wanaoajiriwa NCAA ni watoto/ndugu wa viongozi wakubwa serikalini – wamasai licha ya uzalendo wao wa kulinda rasilimalia wanaachwa bila kupewa kipaumbele cha ajira ( za vibarua na za kudumu), kama sifa ikiwa ni za kitaaluma hakuna mashaka kwamba wapo waliosoma na kustahili kupata nafasi hizo!

Mh Rais Samia wakati wa uzinduzi wa filamu ya Royal Tour ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania – alipata kuiambia Dunia kuwa jamii ya kifugaji hasa ya Ngorongoro ni “Primitive” na kwamba aliogopa kusogelewa na wananchi wakiwa wamevaa kitamaduni wakati wa kuchukua video. Hii haikuwa bahati mbaya, bali ilikuwa ni kuhalalisha kwamba Wamasai ni watu wa hovyo na wanastahili kuondolewa kwenye Maeneo yao. Tulidhani ndimi za Rais anayejali watu wake yasingejielekeza kuhujumu watu wake kwa kuwapa majina mabaya kwani kufanya hivyo ni kujitambulisha kwamba imekosa fikra, na inaongozwa na maslahi ya wachache wenye nguvu ambao wapo kwa ajili ya kupora wananchi mali zao. Tulidhani yeye ni mfariji wa watu wake lakini alituachia maumivu makubwa yasiyomithilika

Ni wakati wa Rais Samia kukiri kuwa fedha za mikopo kutoka Benki ya Dunia na kwa wafadhili mbalimbali yalitumika kufanya kampeni na ujenzi wa mradi wa Msomera Handeni. Wamasai wachache waliohama wameondoka sio kwa uhiyari wao bali Kutokana na nguvu kubwa ya mabavu, vitisho kuwepo dhidi yao. Wapo ambao hadi leo wametolewa na hawajapata fidia hadi sasa licha ya serikali yake Rais Samia kujinasibu kutenda haki. Vilevile kuna mgogoro huko kutokana na mradi kutokuwa shirikishi kwa wenyeji wa Msomera ( mbayo toka hatua za mwanzo hawakushirikishwa – na kwamba maeneo yao yalitwaliwa na kupewa watu wengine toka Ngorongoro) Kwa nini bado kuna usiri wa kutokuambiwa budget ya mradi huu ni kiasi gani? Kwa nini haikupitishwa na Bunge? Kwa nini Rais anakanyaga Katiba? Kwa nini fidia ni siri?

Kuna wakati wa serikali yake wabunge waliishauri kupeleka majeshi na vifaru ili watu waondolewe Ngorongoro kwa nguvu. Kwa nini yeye Rais mwenyewe hakukemea kauli hii? Je ni Kwa sababu yeye ndio aliyebariki yote hayo?

Ni kweli kwamba ingelikuwa wanaondolewa wao au familia yake kwenye eneo lake bado angesifia  na kupongeza? Wafugaji tumechagua kusema ukweli na kwamba hatuoni cha kupongeza dhidi yake zaidi ya kulia kutokana na maumivu yanayofanywa na serikali yake

Kwa Loliondo, operation ilifanyika kati ya 8-10/06/2022 , viongozi wetu walikamatwa 9/06/2022 na kufunguliwa mashtaka ya mauaji 16/06/2022

Baada ya kufanikiwa kukamata watu wetu, wengine waliumizwa , walipigwa na kunyimwa matibabu katika Taifa lao ambayo hulipa kodi pia , waliwafungulia watu kesi za uhamiaji zaidi ya watu 70 , walipora eneo letu na kuanza kuweka bicon tarehe 9.06/2022, na baada uporaji huo wakatoa GN ya Pori haramu la Pololeti 17/06/2022

Longido, mifugo ilipigwa minada Kwa amri ya Serikali, kule Mwanga mtoto wa miaka 17 alipigwa risasi na hatukuona pole ya Rais wala hakuna aliyechukuliwa hatua – Je ni kwamba Wamasai hawana haki ya kuishi?

Miaka miwili ya Rais Samia kwa jamii ya kifugaji imekua ni kilio badala ya furaha, tumenyanyaswa na kuumizwa na serikali yetu wenyewe, mifugo yetu yametaifishwa na kufanywa maskini na serikali yetu , tumefungwa na kuuliwa na serikali ya Mwanamama tuliyedhani angeleta suluhu kwa watu wetu, ni miaka miwili ya kaa la moto

Kosa letu ni kulinda na kutunza uhifadhi, pesa yanayopatikana kwetu yamekua ni sababu ya wao kunufaika, kuwekeza na kutuacha sisi tukiwa ukiwa pasina chochote

Kwako Mheshimiwa Rais ; umekuwa sana Mhubiri wa Haki ingali huishi maneno yako, umekua na maneno matamu yanayokinzana na matendo yao. Unaonesha kuwa uso wa tabasamu – huku sisi tunaona ukiwa mkatili na mpinga haki hasa za watu wasio na nguvu (maskini)

Mh Rais; unahitaji kustawisha nchi yote pasipo kukanyaga haki za wengine, uwekezaji uwe ni wenye kushirikisha wananchi na sio mabavu, uwe ni wenye tija Kwa wananchi ambao ndio waathirika wa Yote hayo

Mh Rais ; uongozi ni kuwajibika pasipo chembe ya ubaguzi kuwaletea watu wote Maendeleo, Maendeleo si Kuhamisha watu Kwa mabavu mliyoivika uhiyari bali ni kuwasikiliza nini wanataka

Nguvu yako ni kubwa kutokana na fedha na vyombo vya ulinzi na usalama yaliyopo ingawa kamwe hautaweza kuzuia wananchi wakiamua kudai haki zao

Ni Mimi Laizer Laizer – mfugaji niliyenyimwa majani, maji na madini joto katika ardhi yangu

Makala hii ni mawazo binafsi ya msomaji wetu ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted