, , , , ,

Hukumu Ya Kesi Ya Uhaini Dhidi Ya Lissu Kuamuliwa Leo

Wadh Kassim Avatar
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, amefikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Novemba 6, 2026, kwa ajili ya kusomewa hukumu katika kesi ya uhaini inayomkabili.
 
Lissu amewasili mahakamani saa 8:23 23 asubuhi, huku kesi hiyo ikisubiriwa kwa karibu na wafuasi wa CHADEMA pamoja na wadau mbalimbali wanaofuatilia mwenendo wake.
 
Hukumu hiyo inatarajiwa kuhitimisha hatua muhimu ya kesi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Lissu alipokamatwa Aprili 9, 2025, mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, kufuatia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliokuwa na kaulimbiu ya No Reforms, No Election.
 
Kesi hiyo inatokana na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambapo upande wa mashtaka unadai kuwa Aprili 3, 2025, Lissu alitoa matamshi yaliyolenga kushawishi wananchi kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17, huku upande wa utetezi ukiwasilisha mashahidi watano, akiwemo Lissu mwenyewe.
 
Wakati wa hoja za mwisho, upande wa mashtaka uliziomba mahakama imtie hatiani Lissu ukidai kuwa ushahidi uliowasilishwa umethibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote ya msingi.
 
Hata hivyo, Lissu alipinga madai hayo, akisisitiza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa linalomkabili na kuiomba mahakama imwachie huru.
 
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Our Correspondent Avatar