Tanzania: Wanafunzi waliopata ujauzito ruksa kurudi shule

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako wanafunzi watakaotaka kurejea shule wataruhusiwa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi

0

Tanzania ilisema Jumatano itawaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo, na kubatilisha sera iliyokosolewa vikali iliyoanzishwa na kiongozi wake marehemu John Pombe Magufuli.

Mnamo mwaka wa 2017, nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilianza kuwafukuza wasichana wajawazito kutoka shule za serikali na kuwapiga marufuku kurejea darasani baada ya kujifungua, katika msako mkali uliopingwa na wanaharakati wa haki.

Kufuatia kifo cha Magufuli mapema mwaka huu, mrithi wake Samia Suluhu Hassan ametaka kuachana na baadhi ya sera zake na Jumatano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa “watoto wa kike waliopata ujauzito wataruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua.”

Mbali na wanafunzi waliopata mimba, wanafunzi wengine waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali nao wataruhusiwa kurejea katika mfumo huo rasmi.

“Nitatoa waraka baadaye leo. Hakuna muda wa kusubiri,”alisema katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu wa Dodoma.

Profesa Joyce Ndalichako, waziri wa Elimu Tanzania

“Takwimu za elimu zinaonyesha kwamba wanafunzi wanaacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoro, ujauzito, vifo pamoja na nidhamu, lakini sababu kubwa katika takwimu za utoro shuleni ambapo kwenye shule za msingi ni 100,008 ambapo wanafunzi watoro ni asilimia 93%, mimba ni asilimia ndogo tu, takribani asilimia 5% ya wanafunzi wanaoacha shule,” alisema waziri Ndalichako.

Magufuli aliapa kuwa hakuna mwanafunzi atakayepata ujauzito na kuendelea na masomo chini ya uongozi wake, akisema ni kinyume cha maadili kwa wasichana wadogo kushiriki kitendo cha ndoa.

“Ninatoa pesa kwa mwanafunzi kusoma bure. Na kisha, anapata mimba, anajifungua na baada ya hapo, anarudi shuleni. Hapana, si chini ya mamlaka yangu,” alisema marehemu John Magufuli mnamo 2017.

Uamuzi huo ulipingwa vikali na vikundi vya watetezi wa haki za binadamu na wafadhili wa kimataifa, ambao walikata ufadhili wao kwa nchi hiyo.

Wakati huo, Human Rights Watch ilichapisha ripoti ikisema maafisa wa shule nchini Tanzania walikuwa wakifanya vipimo vya ujauzito ili kuwafukuza wanafunzi wajawazito, na kuwanyima haki yao ya kupata elimu.

Benki ya Dunia, ambayo ilizuia mkopo wa dola milioni 300 kwa ajili ya elimu ya wasichana ikipinga marufuku hiyo, ilipongeza uamuzi wa Jumatano. “Benki ya Dunia inakaribisha tangazo la serikali ya Tanzania la kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu,” ilisema katika taarifa yake.

Ubalozi wa Uswidi jijini Dar es Salaam, ambao ulikata ufadhili wake kwa Tanzania mwaka jana pia ulipongeza hatua hiyo. “Hii ni hatua nzuri itakayowafaa wasichana wengi, na kuwapa nafasi ya kujiendeleza kikamlilifu” ubalozi ulisema kwenye Twitter.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako wanafunzi watakaotaka kurejea shule wataruhusiwa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi kwa utoro ama kukatiza masomo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted