Shahidi augua ghafla akiwa kizimbani wakati akitoa ushahidi

Ni shahidi wa 10 katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

0

Shahidi wa kumi katika kesi ya Ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu, Inspekta Innocent Ndowo ameugua gafla wakati akiendelea kutoa ushahidi wake akiwa kizimbani.

Inspekta Innocent Ndowo ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya ugaidi ndani yake inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameshindwa kumaliza kutoa ushahidi wake hii leo mahakamani baada ya kuugua ghafla.

Ndowo ambaye ni Inspekta wa Polisi katika kitengo cha Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi katika masuala ya kimtandao ameshindwa kukamilisha kutoa ushahidi wake baada ya kupata tatizo la kiafya.

Awali akitoa ushahidi wake wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Pius Hilla, kabla ya kupata tatizo hilo Ndowo ameiambia Mahakama kuwa yeye kama mtaalamu mwenye ujuzi wa kompyuta na simu za mkononi kwenye kitengo hicho, amekuwa na  jukumu la kupokea vielelezo mbalimbali vinavyohusishwa na makosa ya kimtandao kisha kuvifanyia uchunguzi kulingana na maombi ya taasisi husika inayofanya upelelezi juu ya makosa ya kimtandao.

Shahidi huyo ameendelea kusema kuwa uchunguzi wa vifaa vya kielekroniki ambavyo ni vielelezo unazingatia hatua tatu ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa vielezo husika kwa kutumia vifaa maalumu vya maabara.

Amesema  kuwa Julai Mosi mwaka 2021 Ofisi ya DCI ilimwomba afanye uchunguzi wa miamala ya fedha na mawasiliano ya simu kwenye laini za simu za mtandao wa Airtel na Tigo pamoja na simu nne na kwamba baada ya uchunguzi alibaini laini hizo zilisajiliwa kwa majina ya Freeman Mbowe, Halfan Bwire na Denis Urio.

Shahidi huyo alitaja nyaraka hizo zilizotumika kwenye uchunguzi zenye jina la KYC pamoja na miamala ya fedha kutoka Airtel na kwamba  ina taarifa ya namba za simu ambayo ni . 0784779944, 0782237913 na 0787555200

Kwa mujibu wa shahidi huyo namba 0784779944 ilikuwa ina usajili wa Freeman Aikael Mbowe na namba 0782237913 ilikuwa ina usajili wa Halfan Bwire Hassan na namba 0787555200 ilikuwa na majina ya Denis Leo Urio.

Amedai kuwa uchunguzi wake ulibaini kuwa mnamo tarehe 31/7/2020, namba 0784779944 ilituma fedha kwenda 0782237913 kiasi cha shilingi 80, 000

Akieendelea kutoa ushahidi huo mahakamani hapo Inspekta Ndowo amedai kuwa  baada ya kuandika ripoti juu ya uchunguzi wa vilelezo hivyo ikiwemo barua kutoka Kampuni ya Tigo na Airtel alivikabidhi vielelezo hivyo na ripoti kwa Afande Swila kwa ajili ya hatua nyingine za kiupelelezi.

Hata hivyo wakati shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo alinyoosha mkono mbele ya Mahakama hiyo, na kudai kuwa hayuko sawa kiafya kutokana na maumivu makali ya kichwa aliyokuwa akiyasikia kwa wakati huo.

Kufuatia ombi hilo la shahidi, Jaji anayeendesha kesi hiyo Jaji Jochim Tiganga, ameahirisha kesi hiyo hadi kesho January 18, ambapo shahidi huyo ametakiwa kuja kuendelea kutoa ushahidi wake na endapo hatafika upande wa Jamhuri umetakiwa kuleta shahidi mwingine

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted