Kamati ya PAC Tanzania yabaini hasara ya bilioni 60 ATCL

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Shirika la Ndege (ATCL) lilipata hasara ya shilingi bilioni 60.24 kwa mwaka wa fedha 2019 /2020.

0

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Shirika la Ndege (ATCL) lilipata hasara ya  shilingi bilioni 60.24 kwa mwaka wa fedha 2019 /2020.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Februari 2022, bungeni jijini Dodoma

Amesema katika uchambuzi wa kamati katika taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2020 ulibaini kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilikuwa na mtaji hasi wa shilingi bilioni 246.66 

Aidha  pamoja na changamoto za mtaji, ATCL imekuwa na ongezeko la deni la shilingi bilioni 152. 16 ambapo deni hilo linahusisha shilingi bilioni 70.94 sawa na asilimia 47 ya deni lote, deni ambalo ATCL wanadaiwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).

Naghenjwa amesema  kamati imefanya uchambuzi wa kina katika hesabu zilizokaguliwa za ATCL na kubaini kuwa ATCL ilipata hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 60.24 kwa mwaka wa fedha 2019 /2020 hivyo kufanya hasara jumuifu tangu mwaka 2015/2016 kufikia shilingi bilioni 152.96 .

“Uwepo wa madeni ya muda mrefu ni kihatarishi cha uendelevu wa kampuni kwa siku zijazo. Kwa msingi huo, kihatarishi hicho kimesisitizwa kwa kina katika hati ya ukaguzi iliyotolewa na CAG katika hesabu za ATCL kwa mwaka wa fedha 2019/2020,”amesema.

Kaboyoka amesema suala la msisitizo katika hati hiyo ya ukaguzi ni hoja ya mtaji na madeni ya ATCL hali ambayo inaweza kusababisha kampuni kushindwa kujiendesha kwa siku zijazo.

Amesema hoja nyingine ambazo zinachangia ATCL kutokuwa na ufanisi wa kutosha kifedha hadi sasa na uwepo wa madeni makubwa ya siku za nyuma ambayo hayajalipwa.

Aidha, kuna deni la kiasi cha shilingi bilioni 87.25 bilioni sawa na asilimia 59 ya deni lote, ambalo ni deni la Kampuni ya Wallis Trading Inc. iliyokuwa imeikodishia ATCL Ndege miaka ya nyuma.

Pia walibaini kutofikiwa kwa malengo ya kifedha ya kampuni kwa kiwango cha asilimia ambapo mwaka 2019/2020 ATCL ilipanga kupata mapato kiasi cha shilingi bilioni 661.64.

Hata hivyo, walifanikiwa kupata mapato ya shilingi bilioni 157.60 hali inayoathiri ufanisi wa kampuni.

Kamati hiyo imebaini pia  uwepo wa vifungu kadhaa vya kimkataba ambavyo vinasababisha ATCL kuongeza deni ikiwemo shirika hilo kuingia mkataba wa gharama za ukodishaji wa ndege wa shilingi bilioni 15.46 kati yake na TGFA kutokuwa na kipengele cha vihatarishi visivyotabirika.

Gharama hiyo ilitokana na ukodishaji wa ndege ambazo hazikufanya kazi wakati wa kipindi cha janga la uviko – 19 kati ya Machi 15 na Juni 30, 2020.

Pia kwa mujibu wa Kamati hyo ATCL iliingia gharama mara mbili ya shilingi bilioni 16.97 kama gharama za matengenezo ya ndege kutokana na dosari za kimkataba kati yake na TGFA.

“Masuala hayo matatu kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyochangia kutofikiwa malengo na ufanisi wa ATCL kwa mwaka wa fedha 2019/2020,”imesema taarifa hiyo

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted