Freeman Mbowe akutwa na kesi ya kujibu

Kesi imepangwa kuanza Machi 4, wakati Mbowe na watuhumiwa wengine watakapowasilisha utetezi wao.

0
Freeman Mbowe,Mwenyekiti CHADEMA

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania anakabiliwa na kesi ya ugaidi, jaji wa mahakama kuu alitoa uamuzi huo Ijumaa, katika kesi ambayo wafuasi wake walidai kuwa ni hatua ya kisiasa ya kukandamiza upinzani.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alikamatwa Julai 21 mwaka jana akiwa na baadhi ya viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, katika msako wa usiku wa kuamkia siku ya kongamano la kudai mageuzi ya katiba katika nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 60, ambaye ameshtumu polisi kwa kumtesa karibu miezi saba akiwa kizuizini, alishtakiwa kwa ufadhili wa ugaidi na kula njama.

Baada ya waendesha mashitaka kumaliza kutoa ushahidi dhidi ya Mbowe mapema wiki hii, tetesi ziliongezeka kuwa mahakama ya Dar es Salaam huenda ikamwachia mwanasiasa huyo na hivyo kumaliza sakata lililoibua hali ya demokrasia na utawala wa sheria chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Lakini Ijumaa, Jaji Joachim Tiganga alisema Mbowe na watuhumiwa wengine watatu watatakiwa kujibu mashitaka, uamuzi uliolaaniwa na Chadema.

“Nimetumia siku mbili kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka… Mahakama inaamini kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu,” Hakimu alisema.

Kesi imepangwa kuanza Machi 4, wakati Mbowe na watuhumiwa wengine watakapowasilisha utetezi wao.

Umati wa wafuasi hao wakimshangilia Mbowe wakati akiwasili mahakamani hapo, huku wawakilishi wa mabalozi wa nchi za nje nao wakiwa katika kikao hicho.

Siku mbaya kwa haki

Chadema iliapa itaendelea kupigania “haki” kwa Mbowe.

“Leo ni siku nyingine mbaya katika historia ya haki ya Tanzania,” katibu mkuu wa chama hicho John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Chadema, ambapo yeye na wafuasi wengine walivalia fulana nyeupe zenye maandishi “Hakuna kesi ya kujibu.”

“Haya ni matokeo ya wazi ya kuwa na katiba mbovu ambayo haihakikishii uhuru wa mahakama.”

Kukamatwa kwa Mbowe kulizima matumaini kuwa Samia Hassan angeondoka kutoka katika utawala wa kiimla wa mtangulizi wake John Magufuli, aliyepewa jina la “Bulldozer” kutokana na mtindo wake wa kutobadilika na kuwakandamiza wapinzani.

CHADEMA imeishutumu serikali ya Samia Hassan kwa kuingilia kesi hiyo na kusema kukamatwa huko kunaonyesha nchi ikiingia katika kwa ‘udikteta’.

Katika siku za hivi karibuni hata hivyo, serikali imefanya maamuzi yanayoonekana kuwa ya maridhiano kwa upinzani.

Siku ya Jumatano, Hassan alikutana mjini Brussels na naibu mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye alikuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa urais wa 2020 lakini anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji kufuatia jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017.

Wiki iliyopita, serikali iliondoa marufuku ya miaka mingi iliyowekwa na Magufuli kwa magazeti manne ya Kiswahili, likiwemo Daima — linalomilikiwa na Mbowe.

Waendesha mashitaka walisema tuhuma zinazomkabili Mbowe hazihusiani na kongamano la mabadiliko ya katiba ambalo CHADEMA walipanga kufanya mjini Mwanza Julai mwaka jana, bali ni makosa ya mwaka jana katika sehemu nyingine ya Tanzania.

CHADEMA imesema waendesha mashitaka wanamtuhumu Mbowe kwa kula njama za kumshambulia kiongozi wa umma, na kutoa shilingi Tshs 600,000 ($260, euro 230) kwa ajili ya kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu na kukata miti ili kufunga barabara.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted