Roman Abramovich kuuza Chelsea na fedha kuwanufaisha waathiriwa wa vita Ukraine

Alitangaza kuuzwa kwa klabu hiyo saa moja kabla ya mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Luton, ambapo The Blues walishinda 3-2.

0
Roman Abramovich mmiliki wa klabu ya Chelsea (Photo by Ben STANSALL / AFP)

Mmiliki wa Chelsea Mrusi Roman Abramovich alisema Jumatano amefanya uamuzi ‘mgumu sana’ wa kuiuza klabu hiyo ya Ligi ya Premia, akiahidi kwamba mapato yataenda kwa wahanga wa vita nchini Ukraine.

Bilionea huyo anaamini kuwa ni kwa manufaa ya wachezaji wa klabu kuiuza. Abramovich ameiboresha klabu hiyo tangu alipoinunua mwaka 2003.

Uamuzi wake wa kushangaza unakuja siku chache baada ya Abramovich kusema kuwa anakabidhi udhibiti wa Chelsea kwa wadhamini kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

“Siku zote nimekuwa nikifanya maamuzi kwa nia njema ya klabu,” Abramovich alisema katika taarifa yake.

“Kwa hali ilivyo sasa, nimechukua uamuzi wa kuiuza klabu, kwani naamini hili ni kwa manufaa ya klabu, mashabiki, wafanyakazi, wadhamini na washirika wa klabu.”

Ni wakati wa mabadiliko makubwa kwa soka ya Uingereza baada ya takriban miongo miwili ambapo timu ya Abramovich imekuwa ikishindana mara kwa mara kuwania tuzo ya juu ya mchezo huo.

Chelsea imeshinda mataji 19 makubwa katika enzi ya Abramovich, ikiwa ni pamoja na mataji yao mawili ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na matano ya Ligi Kuu.

Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich akihudhuria mechi kati ya Chelsea na Crystal Palace mnamo Mei 03, 2015 – (Photo by Glyn KIRK / AFP)

Lakini umiliki wa Abramovich mwenye umri wa miaka 55 utafikia kikomo kutokana na mzozo kutoka kwa uvamizi wa Urusi kwa Ukraine.

Abramovich, anayedaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin, hajatajwa kwenye orodha ya vikwazo vya Uingereza inayolenga benki za Urusi, biashara na matajiri wanaounga mkono Kremlin.

Lakini wasiwasi wa mmiliki wa Chelsea kuhusu uwezekano wa kunyakuliwa kwa mali yake unasemekana ulichochea hatua yake ya kuuza klabu hiyo ya The Blues.

Bilionea wa Uswizi Hansjorg Wyss na mwekezaji wa Amerika Todd Boehly, mmiliki mwenza wa timu ya besiboli ya Los Angeles Dodgers, wanaripotiwa kuwa wawili wanaojitayarisha zabuni ya pamoja kuinunua klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Wyss, 86, aliliambia gazeti la Uswizi la Blick kwamba alikuwa amepewa nafasi ya kuinunua klabu hiyo ya London kwa sababu Abramovich alitaka ‘kuiuza Chelsea haraka’ kabla ya kuwekewa vikwazo vya kisiasa.

Inaaminika kuwa bei ya Abramovich kwa Chelsea itakuwa karibu pauni bilioni 3 (dola bilioni 4), huku benki ya Amerika ya Raine Group ikiripotiwa kutakiwa kushughulikia mauzo hayo.

Deni la Chelsea kwa Abramovich kwa sasa linafikia takriban pauni bilioni 1.5 lakini hataomba mkopo huo kulipwa, huku pia akisemekana kuuza mali yake ya London.

Abramovich, ambaye alionekana kushuhudia Chelsea ikishinda Kombe la Dunia la Vilabu huko Abu Dhabi mwezi uliopita, ameahidi kutoa mapato yoyote kutokana na mauzo hayo kusaidia wahasiriwa wa vita nchini Ukraine.

“Uuzwaji wa klabu hautaharakishwa bali utafuata utaratibu unaostahili,” alisema.

“Sitaomba kulipwa mkopo wowote. Hili halijawahi kuwa kuhusu biashara wala pesa kwangu, lakini kuhusu mapenzi dhati kwa mchezo na klabu.”

“Zaidi ya hayo, nimeiagiza timu yangu kuanzisha msingi wa hisani ambapo mapato yote kutokana na mauzo yatatolewa.”Msingi huo utakuwa kwa manufaa ya wahasiriwa wote wa vita nchini Ukraine.

”Hii ni pamoja na kutoa fedha kwa mahitaji ya dharura na ya haraka kwa wahasiriwa, pamoja na kusaidia kazi ya muda mrefu ya kushighilikia wakimbizi.”

Abramovich alilipa pauni milioni 140 kuinunua Chelsea na uteuzi wa kijanja wa Jose Mourinho kama meneja ulisaidia kuvishinda vilabu vya Manchester United na Arsenal.

Alitangaza kuuzwa kwa klabu hiyo saa moja kabla ya mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Luton, ambapo The Blues walishinda 3-2.

Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel alisema “Nadhani kila uamuzi anaochukua (Abramovich) ni uamuzi sahihi, ni chaguo lake, klabu yake, si juu yangu kutoa maoni,” aliiambia BBC.

Abramovich alisema anatumai kufanya ziara ya mwisho uwanjani Stamford Bridge kuwa aga wachezaji.

“Tafadhali fahamu kuwa huu umekuwa uamuzi mgumu sana kufanya, na inanitia uchungu kuachana na klabu kwa njia hii,” alisema.

Aliongeza: “Imekuwa faraja kwangu kuwa sehemu ya Chelsea FC na ninajivunia mafanikio yetu yote ya pamoja. Klabu ya soka ya Chelsea na wafuasi wake watakuwa moyoni mwangu daima.”

Roman Abramovich mmiliki wa klabu ya Chelsea (Photo by Ben STANSALL / AFP)
In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted