Tulimlipa Ruto mabilioni kumuunga mkono Rais Kenyatta, Tuju afichua

Mkurugenzi Mtendaji wa sekretarieti ya urais ya Azimio, Raphael Tuju ameibuka na ufichuzi wa kushtua kwamba DP Ruto alilipwa mabilioni ili kuungana na Rais Kenyatta katika uchaguzi wa...

0
Raphael Tuju, Mkurugenzi Mtendaji wa sekretarieti ya Azimio

Dhana kwamba Naibu Rais William Ruto alimuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta bila masharti katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 sasa imetiliwa shaka.

Hii ni baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa sekretarieti ya urais ya Azimio, Raphael Tuju kuibuka na ufichuzi wa kushtua kwamba DP Ruto alilipwa mabilioni ili kuungana na Rais Kenyatta katika uchaguzi wa 2013.

“Watu wengi waliomuunga mkono Rais Uhuru walijitolea kukusanya pesa hizi ili Ruto uangane na Uhuru….Kwa mtu anayesema KSh7 Bilioni pekee, dhana yako ni sawa na yangu lakini ilikuwa mabilioni, ” Tuju alisema katika mahojiano.

Tuju alifichua kuwa pesa hizo zililipwa kama malipo ya kwanza kabla ya uchaguzi huku malipo mengine yakifanywa kupitia udhibiti wa hati kuu za wizara ndani ya utawala wa Jubilee.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee alidai kuwa Ruto alipoingia madarakani alihusika na uporaji haraka.

“Zimesalia siku 12 twende kwa uchaguzi na Wakenya wanahitaji kujua ukweli,

“Sijui ni kwa nini watu kutoka kati wanafikiri kuwa kuna  chochote wanasthaili kumlipia ilhali alilipwa na kulikuwa na masharti ya yeye kupokea pesa hizi mapema,” alisema.

Tuju alimwondolea Rais Kenyatta makosa yoyote kwa kuamua kuungana na DP Ruto akisema ilikuwa suala gumu na hawakuwa na budi.”

“Rais Uhuru Kenyatta alikuwa kati ya papa na mamba.

Upande mmoja alikuwa Raila mwingine alikuwa Ruto ambao walikuwa tayari kumla.

Kwa hivyo, ilibidi achague ni nani kati ya hao hatamla na kummaliza,” Tuju alifichua.

“Ndio, ikiwa ni lazima kwangu kurudia jambo hili katika mahakama ya sheria, basi nitafanya hivyo kwa sababu najua nina ushahidi na sio mimi pekee mwenye ushahidi,” aliongeza.

Tuju alimtaja DP Ruto kama mtu asiyefaa kushikilia wadhfa wa urais akisema sifa na mwenendo wake katika utawala wa Jubilee unaonyesha kuwa ni kiongozi mfisadi.

Alibainisha kuwa tuhuma za unyakuzi wa ardhi na ufisadi zinazomkabili Naibu Rais hazikuwa propaganda tu.

“Kutokana na ulaghai aliokuwa akitupitishia na suala la Arror na Kimwarer ambapo bei iliongezwa mara kumi nukta moja inafikia mahali ambapo huwezi kukubali ufisadi wake tena.”

Kila mtu anashangaa kilichotokea ili Uhuru awasiliane na Odinga,” akasema.

Haya yalijiri huku kukiwa na hisia kutoka kwa DP Ruto kwamba alimuunga mkono bosi wake bila masharti na hatua ya Uhuru ya kumuunga mkono Raila Odinga kama mrithi wake sio kitendo cha usaliti.

“Nataka kusema ili kuepuka shaka kwamba nilimuunga mkono rafiki yangu si kwa sababu ya jamii yake si kwa sababu ya lugha anayozungumza. Simdai Uhuru chochote na hana deni lolote na jamii yetu,” Ruto alisema Januari, 2021.

Rais Kenyatta na naibu wake sasa wamegeuka kuwa maadui kwa kurushiana matusi katika wiki chache zilizopita huku siasa za 2022 zikipamba moto, huku Kenyatta akitangaza hadharani kwamba hatamruhusu Ruto kumrithi.

Kenyatta anampigia debe kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ambaye anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Azimio La Umoja One Kenya Party.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted