Nitatafuta haki kwa njia ya amani, asema kiongozi wa Azimio Raila Odinga

Kiongozi wa Azimio la umoja raila Odinga amewataka wakenya kudumisha amani wakati akiendelea kutatafuta haki mahakamani.

0
Viongozi wa Azimio la umoja Raila Odinga, Martha Karua na Kalonzo Musyoka.

Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Kenya Raila Odinga amesisitiza kuwa ataelekea mahakamani kutafuta haki ya ushindi aliyopokonywa na kuwataka wakenya kuendelea kudumisha amani.

Kiongozi huyo amewaambia viongozi wa kidini ambao walimtembelea nyumbani kwake katika mtaa wa Karen jumamosi ya leo kuwa anaamini uchaguzi haukuwa wa uwazi, huru na haki.

“Mwafahamu kilichotokea katika ukumbi wa Bomas, hiyo haikuwa uchaguzi kwa kuwa haikuandaliwa kwa njia ya uwazi. Tutakwena mahakamani kutafuta haki na kuhakikisha kuwa ulimwengu nzima unafahamu kilichokea,” alisema Odinga.

Odinga amepuuzilia mbali tangazo la tume ya uchaguzi na mipaka kenya IEBC kumfanya William Ruto kuwa rais mteule akisema ni kwa muda tu.

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga

“Bado hakuna rais mteule nchini Kenya,unaposkiza makamishna wanne waliojitenga na matokeo ya Chebukati utafahamu kuwa  kuna tatizo tena kubwa sana,” aliongeza Odinga.

Kwa mujibu wa katika ya Kenya, yeyote anayepinga matokeo yaliotangazwa na tume ya IEBC tarehe 15 mwezi agosti anafaa kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo hayo kufikia siku ya jumatatu.

Hata hivyo habari kutoka kwa washirika wakuu  wa kiongozi wa  muungano wa Azimio Raila Odinga zinaashiria watawasilisha kesi katika mahakama ya juu zaidi siku ya jumatatu.

Kulingana na sheria kesi hiyo inafaa kuskizwa na kuamuliwa ndani ya siku 14 kuanzia siku iliyowasilishwa na iwapo itatupiliwa mbali basi rais mteule William Ruto ataapishwa kama rais wa tano wa Kenya.

Lakini ikibatisha kuchaguliwa kwa Ruto, mahakama hiyo itaamrisha kufanyike marudio ya uchaguzi.

Tangu mwaka 2002, chaguzi zote Kenya zimekuwa zikipingwa na kiongozi wa Azimio bwana Odinga anasema aliibiwa ushindi wake katika chaguzi za mwaka 2007, 2013 na 2017.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted