Raila Atoa Makataa Ya Siku 14 Kwa Serikali Ya Rais Ruto Kupunguza Gharama Ya Maisha nchini Kenya.

Odinga ambaye siku ya Jumatano Februari 22 aliandaa mkutano wa maombi katika bustani ya Jeevanjee jijini Nairobi alisema kuwa wakenya wamechoka na serikali ya Kenya Kwanza kutotimiza ahadi...

0

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amempa Rais William Ruto makataa ya siku 14 kuhakikisha kuwa amepunguza gharama ya maisha.

Odinga ambaye siku ya Jumatano Februari 22 aliandaa mkutano wa maombi katika bustani ya Jeevanjee jijini Nairobi alisema kuwa wakenya wamechoka na serikali ya Kenya Kwanza kutotimiza ahadi walizotoa katika kipindi cha kampeni.

“Tumekuwa tukizungumzia sana kupanda kwa bei ya bidhaa kama unga,umeme na mafuta.Tumelalamika kuhusu kuongezeka kwa ushuru na hivi majuzi tukaangazia ongezeko la visa vya wanafunzi kulazimika kuwacha shule kutokana na ukosefu wa karo” alisema Odinga.

“Kutolewa kwa ruzuku ya chakula na elimu wakati ukame na baa njaa linaathiri taifa ulikuwa uamuzi ambao hauna utu kabisa.Tunataka sasa ruzuku hizi kurejeshwa na bei ya bidhaa na ushuru kupunguzwa ndani ya siku 14 zijazo” alisema Odinga.

Kiongozi huyo wa upinzani nchini kenya alidokeza kuwa iwapo serikali ya rais William Ruto itakaidi onyo lao,mrengo wa azimio utawakusanya wafuasi wake na kuandaa maandamano kote nchini.

Odinga hata hivyo ameitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini kenya IEBC kuruhusu wakaguzi kudurusu sava zao zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022.

“Udanyanyifu katika uchaguzi lazima ufikie kikomo.Sava za IEBC lazima zifunguliwa na kukaguliwa,wananchi wanataka kupata haki yao kwani walijitokeza kwa wingi kutupigia kura” alisema Odinga.

Viongozi wa Azimio hata hivyo wanataka sasa kujumuishwa katika mchakato wa kuwateua makamishna sita wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini kenya (IEBC) baada ya watatu kujiuzulu na muhula wa wengine watatu kutamatika.

“Mchakato wa kuwateua makamishna wa IEBC unafaa kusimamishwa.Jopo lisilo na mapendeleo linafaa kuwekwa pale ili kuweka miundo msingi sawa katika IEBC.Kila upande unafaa kuhusishwa katika mchakato huu.” alisema Odinga.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted