#KENYA: Idadi ya vifo katika ibada ya Shakahola imeongezeka hadi 83

Kiongozi huyo wa madhehebu alikamatwa Aprili 14 kufuatia taarifa iliyodokeza kuwepo kwa makaburi mafupi yenye miili ya baadhi ya wafuasi wake

0
Mchungaji Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International Church huko Shakahola, Malindi, Kenya. Aliwataka wafuasi wake wafe kwa njaa ili wakutane na Yesu, wote walikufa na kuzikwa katika makaburi ya siri

Polisi walipata miili 10 zaidi msituni huko Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Jumanne asubuhi, na kufanya jumla ya waliofukuliwa kufikia 75, watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa dhehebu la Kikristo ambao waliamini kuwa wangeenda mbinguni ikiwa watakufa njaa.

Jumla ya vifo vinavyotokana na dhehebu hilo linaloongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie sasa inafikia 83, wakiwemo wahasiriwa wanane waliokufa baada ya kuokolewa katika msako wa polisi ambao uliondoa mfuniko wa hofu katika kanisa hilo.

Polisi pia waliwaokoa wanawake wawili ambao walikuwa na utapiamlo mkali na walionekana kukaribia kufa. Walikimbizwa katika hospitali ya Malindi kwa matibabu.

Kati ya miili 10 iliyopatikana Jumanne asubuhi, mitano ilipatikana ikiwa imezikwa katika kaburi moja huku mingine mitano ikiwa katika maeneo tofauti.

Wapelelezi wa mauaji tangu wiki jana wamekuwa wakitafuta makaburi kwenye eneo la ekari 800 la Mackenzie.

Kiongozi huyo wa madhehebu alikamatwa Aprili 14 kufuatia taarifa iliyodokeza kuwepo kwa makaburi mafupi yenye miili ya baadhi ya wafuasi wake.

Mackenize, kiongozi wa kanisa la Good News International Church, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Malindi Elizabeth Usui mnamo Aprili 17 na hakutakiwa kujibu shtaka lolote, huku upande wa mashtaka ukitaka siku 30 zaidi za kumzuilia watakapokamilisha upelelezi. Mahakama iliwapa polisi siku 14.

Alifikishwa mahakamani pamoja na watu wengine 13 katika kesi hiyo itakayotajwa Mei 2.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted