Mabomu ya machozi, kukamatwa na polisi, huku Wakenya wakipinga ongezeko la ushuru

Odinga alitangaza mipango ya kukusanya saini milioni 10 kwa nia ya kumwondoa afisini Rais William Ruto

0
Wafuasi wa upinzani wakiwa na mabango yenye maandishi ‘Tumechoka’ wanaposhiriki katika mkutano wa hadhara wa kupinga gharama ya juu ya maisha baada ya kupitishwa kwa mswada wa fedha katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi, Kenya Julai 7, 2023. (Picha na Luis Tato/AFP )

Polisi wa Kenya walirusha vitoa machozi kwenye msafara wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga siku ya Ijumaa huku mashirika ya kutetea haki ya binadamu yakilaani “kukamatwa kiholela” wakati wa maandamano ya kuipinga serikali kuhusu mgogoro wa gharama ya maisha na msururu wa ongezeko la kodi lenye utata.
Vitoa machozi vilirushwa kwenye msafara wa Odinga baada ya kuhutubia katika mji mkuu Nairobi.

Polisi walichukua hatua sawa na hivyo kuvunja maandamano katika mji wa Mombasa na Kisumu, ngome ya upinzani kwenye Ziwa Victoria magharibi mwa Kenya.

Polisi pia walikamata watu kadhaa jijini Nairobi, huku ulinzi ukiimarishwa kwa maandamano ya hivi punde zaidi yaliyoitishwa na Odinga mwaka huu dhidi ya sera za serikali ya Rais William Ruto.

Katika mkutano huo, Odinga alitangaza mipango ya kukusanya saini milioni 10 kwa nia ya kumwondoa afisini mpinzani wake mkuu.

“Wakenya walichagua viongozi bungeni na wamewasaliti,” alisema huku akishangiliwa. “Ruto mwenyewe ambaye alichukua mamlaka kinyume cha sheria amewasaliti Wakenya.”

Muungano wa Azimio wa Odinga ulikuwa umeitisha maandamano kuhusu athari za ushuru mpya kwa Wakenya ambao tayari wanatatizika kiuchumi na kupanda kwa bei ya mahitaji ya kimsingi.

Wiki jana, Ruto alitia saini kuwa sheria mswada wa fedha unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya dola bilioni 2.1 kwa hazina ya serikali iliyopungua na kusaidia kukarabati uchumi uliokumbwa na madeni makubwa.

Sheria ya Fedha inatoa ushuru mpya au ongezeko la bidhaa mbalimbali za kimsingi kama vile mafuta na chakula na uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, pamoja na ushuru wenye utata kwa Wakenya wote wanaolipa ushuru kufadhili mpango wa nyumba.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted