Kenya: Tume ya IEBC yamtaka Sabina Chege kufika mbele yake

Kauli ya tume ya uchaguzi inajiri baada ya Chege kudai kuwa chama cha Jubilee kilishinda uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya kuiba kura

0
Sabina Chege,Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imemwita Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege kutokana na matamshi aliyoyatoa kwenye mkutano wa hadhara katika Kaunti ya Vihiga.

Katika taarifa iliyotolewa na IEBC mnamo Ijumaa, Februari 11, ilifichuka kuwa mbunge huyo alihitajika kufika mbele ya Kamati ya Tume ya Maadili mnamo Jumanne, Februari 15.

Kauli ya tume ya uchaguzi inajiri siku moja tu baada ya Chege kudai kuwa chama cha Jubilee kilishinda uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya kuiba kura

“Unatakiwa kufika katika Ofisi za Tume katika jengo la Anniversary Towers Jumanne, Februari 15 saa 0900 saa za mchana kwa ajili ya kuchunguzwa na Tume ya Maadili ya Uchaguzi,” ilisoma barua hiyo kwa Chege, iliyotiwa saini na Katibu, Kamati ya Utekelezaji wa Maadili ya Uchaguzi.

Baada ya mkutano wa Vihiga, kulizuka tafrani kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wakitaka vyombo vya uchunguzi kumchukulia hatua mbunge huyo ili kuweka rekodi sawa.

Viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wamemkashifu Chege kwa maoni yake huku wakitahadharisha baraza la uchaguzi dhidi ya kuunga mkono upande wa mpinzani katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wakati wa mkutano wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Nakuru mnamo Ijumaa, Februari 11, Ruto alipuuza madai yaliyotolewa na Chege akisema kuwa utawala wa Jubilee ulishinda uchaguzi wa 2017 kwa haki.

“Kuna mtu kutoka Azimio alisema kuwa mimi na Uhuru tuliiba uchaguzi 2017. Nataka kuwauliza nyinyi watu wa Nakuru, je, kura zenu ziliibiwa? Hamkutupigia kura?”

“Hatukuiba kura za mtu yeyote. Watu wa Azimio wakome kutishia watu kwa tuhuma za wizi wa kura. Nilikuwa msimamizi wa uchaguzi na Uhuru hakuiba kura za mtu yeyote,” Ruto alisema.

DP pia alisema kwamba watahakikisha kuwa uchaguzi wa Agosti 9 unakuwa huru na wa haki na matokeo ya uchaguzi hayaathiriwi kwa njia yoyote.

Chege bado hajatoa taarifa kujibu mwito wa IEBC au kuzungumzia matamshi yake katika mkutano wa hadhara mjini Vihiga mnamo Alhamisi, Februari 10.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted