Rais Samia agusia tena matukio ya mauaji nchini Tanzania

Asisitiza viongozi wa dini na machifu kuirejesha jamii karibu na Mungu kuondoa imani potofu

0
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba viongozi wa dini pamoja na machifu kusaidia kuirejesha jamii karibu na Mungu ili kuondoa wimbi la mauaji ya raia ambalo linaendelea hapa nchini.  

Akizungumza katika maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya Askofu Severine Niwemugizi katika viwanja vya Posta – Ngara Mjini, mkoani Kagera, Rais Samia amekiri uwepo wa vitendo vya mauaji na kujiua kwa raia katika maeneo mbalimbali nchini, huku akisema kuwa nyoyo za watu hivi sasa zimekosa hofu

“Kumekuwa na Matukio mengi ya mauji na watu kujiua kwa kipindi hiki.Takwimu zinaonesha katika wilaya ya Ngara (mkoani Kagera) pekee mwaka 2020 kulikuwa na matukio 22 ya mauaji, Mwaka 2021 (21), Mwaka 2022 kulikua na matukio matatu ya watu kujiua.

Rais Samia amesema serikali imekuwa ikiunda tume ndani ya jeshi la polisi kuchunguza sababu za mauaji hayo. Hata hivyo taarifa za uchunguzi zimekuwa zikionesha chanzo kikiwa ni mapenzi, ugumu wa maisha, imani za kishirikina na mambo mengine.

“Lakini ukiangalia  sababu zote hizi, wizi wa mapenzi, kuwania mali, kulipana visasi, imani za kishirikina, ugomvi wa kifamilia na msongo wa mawazo … sababu zote hizi zinaonesha watu hawako karibu na mungu. Amesema Rais Samia na kuongeza kuwa 

“Hakuna dini inayotoa ruhusa kufanya hayo. Anayetoa uhai ni mungu peke yake. Tunafunzwa kuamini kwamba kifo kinapotokea ni kazi ya mungu.”

Rais Samia amedai kuwa kama Chifu Mkuu, Machifu wana kazi nyingine tena kusaidia serikali kutokomeza tatizo hilo.

“Tunakazi kubwa ya kufanya tena hapa. Machifu mnaaminiwa sana na jamii zinazo wazunguka. Tuna kazi kubwa ya kuwaambia watu wanachokifanya kinachotokea sicho tulicho amrishwa kwa dini wala mila na desturi zetu. Hakuna mila na desturi zinazo amrisha watu wakauwane. Hili ni jukumu letu sote watanzania,” amesema Rais Samia.

Aidha  Rais Samia amesema kwa upande wa Serikali inakusudia kutumia somo la urai linalofundishwa kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kote nchini kutoa elimu kuwaepusha wananchi kuanzia ngazi ya chini kuepuka kujiingiza katika vitendo vya kujiua ama kuua.

  “Serikali tutajipanga ratiba hizi zianzie mashuleni. Na kwa bahati nzuri tuna somo la uraia, hilo ndio somo tutakalopenyeza mambo haya yafundishwe kwa watoto,” alisisitiza Rais Samia.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted