Dkt. Ndumbaro: EXPO2020 Dubai yaiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro amesema Maonesho ya Kibiashara ya Expo2020 Dubai yanazidi kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia

0

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro amesema Maonesho ya Kibiashara ya Expo2020 Dubai yanazidi kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kutokana na Watu wa Mataifa mbalimbali Duniani kujua Hifadhi za Tanzania ikiwemo Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro, Madini ya Tanzanite, Mlima Kilimanjaro yapo Tanzania na sio nchi jirani.

Hatua hiyo inakuja kufuatia upotoshwaji wa muda mrefu ambao umekuwa ukifanya na baadhi ya nchi za jirani kuwa kila vivutio vizuri vya utalii ambavyo vipo Tanzania huwahadaa watalii kuwa vipo nchini mwao.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo leo ambapo amedai kuwa watu mbalimbali ambao wamekuwa wakitembelea Banda la Tanzania wamekuwa wakishangaa kuona madini ya Tanzanite, Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro pamoja na Hifadhi ya NgoroNgoro kuwa zipo Tanzania.

” Nimekuwa nikizungumza na wageni mbalimbali wanaotembelea Banda ka Tanzania wengi wao wamekuwa wakishangaa na kukiri kuwa mwanzo walikuwa wanajua kuwa vivutio hivyo havipo Tanzania bali vipo nchi jirani” alisema Dkt. Ndumbaro

Ameongeza kuwa “Maonesho haya ya Dubai yameipaisha Tanzania kuwa ni nchi yenye utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii ambavyo ni vizuri tofauti na wenzetu wanaopotosha kuwa ni vyao” alisisitiza Dkt. Ndumbaro.

Miongoni mwa taasisi za Tanzania za Wizara ya Maliasili na Utalii zinazoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyanapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS).

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza Oktoba Mosi mwaka 2021 yanaendelea hadi Machi 31 mwaka huu na yameshirikisha zaidi ya nchi 192.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted