Mwenyekiti wa BAZECHA, akamatwa tena na polisi nchini Tanzania

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Tanzania(DPP), Sylvester Mwakitalu leo amemuomdolea mashitaka ya uchochezi Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Hashimu Juma, yaliyokuwa yanamkabili ya uchochezi kupitia kifungu cha...

0
Hashim Juma Issa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Tanzania(DPP), Sylvester Mwakitalu leo amemuomdolea mashitaka ya uchochezi Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Hashimu Juma, yaliyokuwa yanamkabili ya uchochezi kupitia kifungu cha 90 (1), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam

Mzee Hashim Juma Issa (63), alikamatwa na polisi mnamo Oktoba 3,2021 akiwa nyumbani kwake huko Unguja visiwani Zanzibar na watu waliojitambulisha kuwa ni maaskari polisi licha ya kuwa hawakumuambia wanakwenda nae wapi siku hiyo.

Baada ya kusambaa kwa taarifa ya kukamatwa kwake Jeshi la polisi lilithibitisha kumshikilia ambapo Oktoba 4,2021 alisafirshwa hadi jijini Dar es salaam kwa maohijiano zaidi na jeshi hilo

Oktoba 7, 2021 Mzee Hashimu alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam, na kusomewa mashitaka mawili na Wakili wa Serikali Yusuph Abood mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Abood siku hiyo alidai mahakamani kuwa, Oktoba Mosi katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alisambaza taarifa kwa lengo la kumchafua na kumdhalilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

Alidai mshtakiwa alichapisha kwenye kompyuta na kusambaza taarifa kuwa “Sirro ni gaidi namba moja nchini Tanzania na fisadi.”

Ilidaiwa katika shitaka lingine kuwa Oktoba Mosi katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alitoa maneno ya uchochezi kuwa “Sirro ni gaidi namba moja nchini Tanzania na fisadi” kwa lengo la kutengeneza chuki kwa wananchi.

Baada ya mshitakiwa kusomewa mashtaka yake, mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo, hivyo aliachiwa kwa dhamana siku hiyo baada ya kutakiwa kuwa na wadahamini wawili waliosaini bondi ya shilingi milioni tatu kila mmoja, barua ya utambulisho pamoja na kitambulisho cha taifa.

Kesi hii imetajwa mahakamani hapo kwa takribani miezi 4 sasa, lakini hii leo iliitwa tena kwa ajili ya kutajwa, lakini  wakili wa Serikali aliieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea nayo tena.

“Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini DPP hana nia tena ya kuendelea na shauri hili kwa mujibu wa kifungu cha 90(1) cha CPA”

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wa utetezi Hekima Mwaisipu, uliiambia mahakama kuwa hawana pingamizi na hoja hiyo iliyowasilishwa mahakamani hapo isipokuwa wameiomba Mahakama kuwa mara baada ya mteja wake kuachilia basi asisumbuliwe tena.

Hata hivyo mara baada ya Mahakama kumalizana na shauri hilo nje ya mahakama hiyo Polisi walimkamata tena Mzee Hashimu, akiwa anatoka mahakamani huku wakimwambia kua ni maelekezo kutoka juu.

Kwa mujibu wa Wakili Mwaisipu Mzee Juma mara baada ya kukamatwa amepelekwa Kituo cha kati cha Polisi(Central Police Dar es salaam)

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted