‘Mbakaji wa Facebook’ Thabo Bester afikishwa katika mahakama ya Afrika Kusini

Bester na wenzake walikamatwa nchini Tanzania wakiwa na hati kadhaa za kusafiria.

0
Mbakaji na muuaji aliyehukumiwa kutoka Afrika Kusini Thabo Bester akitazama wakati akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bloemfontein Aprili 14, 2023. (Picha na – / AFP)

Mbakaji na muuaji Thabo Bester ambaye alitoroka jela na kuacha maiti iliyoungua ndani ya seli yake, alifikishwa katika mahakama ya Afrika Kusini siku ya Ijumaa, siku moja baada ya kurejeshwa kwa ndege kutoka Tanzania.

Bester, ambaye kutoroka kwake gerezani kumetawala nchi kwa wiki kadhaa, alifika katika chumba cha mahakama, akiwa amevalia suti ya rangi ya njano huku miguu na mikono yake ikiwa imefungwa pingu.

Bester, 37, alilindwa vikali katika mahakama ya Bloemfontein karibu kilomita 400 kusini magharibi mwa Johannesburg, akiwa amezingirwa na polisi wengi.

Aliyepewa jina la “mbakaji wa Facebook”, Bester, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani mwaka wa 2012, aliwarubuni waathiriwa kwenye mtandao huo wa kijamii kabla ya kuwabaka na kuwaibia. Aliua angalau mwathirika mmoja.

Alitoroka kutoka kwa gereza la kibinafsi karibu mwaka mmoja uliopita, lakini polisi walisema waligundua mwezi uliopita.

Mnamo Mei 2022, mwili wa mwanamume uliochomwa moto ulipatikana katika seli ya Bester, na kusababisha wakuu wa magereza kuamini kuwa alijichoma moto, lakini DNA baadaye ilifichua mwili huo ulikuwa wa mtu mwingine.

Bester alikamatwa Ijumaa iliyopita na polisi wa Tanzania, baada ya kutoroka Afrika Kusini pamoja na anayedaiwa kuwa mpenzi wake Nandipha Magudumana na mshirika wa Msumbiji.

Magudumana, ambaye ni daktari maarufu alifikishwa mahakamani Alhamisi akikabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwemo mauaji.

Ombi la Bester kuhutubia mahakama lilikataliwa na hakimu.

Wakili wake alisema Bester hakuwa amekula kwa zaidi ya saa 24 na angekubali tu chakula kinachotolewa na timu yake ya wanasheria, akitaja hofu na maswala ya usalama.

Wakili wa Bester aliomba arejeshwe mahakamani haraka iwezekanavyo, lakini walishindwa kwa vile serikali ilisema ilihitaji mwezi mmoja kufanya uchunguzi na kuhakikisha itifaki za usalama zipo kwa Bester kufikishwa mahakamani tena.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 16.

Waziri wa Masuala ya Ndani Aaron Motsoaledi aliambia mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba idara haikuweza kufuatilia maelezo muhimu ya utambulisho wa Bester.

Motsoaledi alisema Bester “hayupo katika mfumo wetu”, akiongeza kuwa hakuwa na kitambulisho, cheti cha kuzaliwa au pasipoti iliyotolewa na idara.

Bester na wenzake walikamatwa nchini Tanzania wakiwa na hati kadhaa za kusafiria.

Wengine wanne wamekamatwa hivi karibuni kuhusiana na mpango wa kutoroka akiwemo babake mganga huyo.

Magudumana na wenzake wanne watafikishwa mahakamani Aprili 17.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted